Kombe la Dunia 2018: Ufaransa mabingwa wa dunia baada ya kuwacharaza Croatia 4-2

Ufaransa iliyoingia mechi hiyo ikisaka ubingwa wa dunia kwa mara ya pili tangu 1998, ilitangulia kwenye mechi na goli la kwanza dakika ya 18 kufuatia mkwaju wa Antoine Griezmann ulioelekezwa wavuni na Mario Mandzukic.

Mandzukic, shujaa dhidi ya Uingereza nusu fainali kwa kuipa goli la ushindi muda wa ziada, alimiminiwa lawama kwa kujifunga na kuwa mchezaji wa kwanza kupiga mpira hadi lango lake katika fainali ya Kombe la Dunia.

Uongozi wa Ufaransa ulidumu kwa dakika 10 pekee kwani winga matata wa Croatia anayeichezea Inter Milan Ivan Perisic, alifyatua kombora ndani ya sanduku na kukatiza sherehe za Ufaransa.

Pande zote zilionyesha dalili za kutofungana hadi dakika ya 37 pale Perisic alipounawa mpira wa kupinda wa Antoine Griezmann na kusababisha penalti.

Mfungaji Griezmann hakuchelea kuipa Ufaransa uongozi kwa kumduwaza kipa wa Croatia Subasic aliyeng'aa kwa kupangua matuta mechi za awali dhidi ya Denmark na Urusi.

Magoli ya Paul Pogba na Kylian Mbappe kipindi cha pili yaliikabidhi Ufaransa Kombe la Dunia mbele ya rais wake Emmanuel Macron na maelfu ya mshabiki ugani Luzhniki.

Kylian MbappeHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionMbappe amekuwa kama Pele (1958) kufunga bao fainali Kombe la Dunia akiwa hajatimiza miaka 20

Baada ya kutolewa hatua ya makundi 2002, kufungwa na Italia 2006 kwenye fainali, kukumbwa na sakata kikosini 2010, na kutemwa na Ujerumani katika robo fainali 2014, hatimaye the Blues, chini ya Didier Deschamps wamefanikiwa jaribio lao Urusi 2018 kwa kuikung'uta Croatia 4-2 muda wa kawaida.

Presentational white space

Mabao yalivyofungwa

  • Ufaransa 1-0 Croatia Mario Mandzukic: bao la kujifunga dakika ya 18
  • 1-1 Ivan Perisic dakika ya 28
  • 2-1 Antoine Griezmann: Penalti dakika ya 38
  • 3-1 Paul Pogba: dakika ya 59
  • 4-1 Kylian Mbappe: dakika ya 65
  • 4-2 Mario Mandzukic: dakika ya 69
Presentational white space

Safu ya Croatia ikiongozwa na Luka Modric ilijitahidi kusawazisha kipindi cha pili lakini ukuta wa Ufaransa, uliojengwa kwa Samuel Umtiti wa Barcelona na Raphael Varane wa Real Madrid ulitoa ulinzi wa kutosha kwa mdakaji Lloris na wavu wake.

Timu hizi zilizidisha ushambulizi lakini ni bidii ya Ufaransa iliyotuzwa kwa bao la Paul Pogba dakika ya 59.

France celebrate winning the World CupHaki miliki ya pichaCLIVE ROSE

Kinda Kylian Mbappe alitonesha kindonda cha Croatia dakika ya 65 kwa kupachika la nne la Ufaransa kujaa kambani na kujiweka kwa vitabu vya historia kuwa chipukizi wa Pili baada ya miaka 60 kujipa goli fainali ya Kombe la Dunia.

Mbappe alitunukiwa medali ya chipukizi bora Kombe la Dunia Urusi.

Antoine Griezmann (France)Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionGriezmann amewafungia Ufaransa mabao 10 katika mashindano makubwa

Kwa mara nyingine, Croatia ilikaribia kufupisha sherehe za Ufaransa kwani mfungaji Mandzukic alijinufaisha kwa kosa la kipa Lloris dakika ya 69 na kufufua matumaini ya Croatia.

Ufaransa iliimarisha ngome yake dakika 20 za mwisho mna kushikilia uongozi wake hadi refa alipopuliza kipenga cha mwisho.

Licha ya kuwa katika timu iliyolazwa kwenye fainali, juhudi za nahodha wa timu hiyo Luka Modric hazikusahaulika kwani amekabidhiwa mpira wa dhahabu kwakuwa mchezaji bora wa Kombe hili.

Mwingine aliyetunukiwa ni kipa wa Ubelgiji Thibaut Coutois aliyenyakua tuzo ya glavu za dhahabu kwa kuwa mdajaki bora Urusi.

Ingawa Uingereza ilimaliza nafasi ya nne, mfungaji wake Harry Kane alitia kapuni kiatu cha dhahabu kwani mabao ya Mbappe ya Griezmann hayakufikia sita aliyofunga Kombe hili

Maoni